Research Papers

Browse

Recent Submissions

Now showing 1 - 2 of 2
  • Item
    Hatima ya maisha ya Waafrika katika Bunilizi za Kiswahili: Mwegamo wa kifalsafa
    (Ruaha Journal of Arts and Social Sciences (RUJASS), 2021) Duwe, Martina
    Makala hii imefafanua sababu za hatima ya maisha ya mwanadamu kulingana na fikra za Waafrika kwa kurejelea riwaya za Utengano (1980) na Tata za Asumini (1990). Data za msingi zilizofafanuliwa katika makala hii zimepatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji makini. Nadharia ya Udhanaishi imetumika kama mwegamo muhimu katika uchambuzi na mjadala wa data zilizowasilishwa katika katika utafiti uliofanyika. Matokeo yanaonesha kuwa utajiri wa maarifa yaliyomo ndani riwaya teule husawiri maudhui na fikra halisi za Waafrika kulingana na tamaduni zao. Fikra hizo hudhihirisha falsafa inayotawala maisha yao. Pia, hubainisha sababu mbalimbali za hatima ya mwanadamu kulingana na mitazamo ya Waafrika. Kifo ni miongoni mwa sababu zilizobainika wazi katika riwaya teule kuwa kinasababishwa na maamuzi ya Mungu, maovu ya mwanadamu mwenyewe na watu wanaomzunguka katika mazingira yake halisi; na namna Waafrika wanavyofikiri juu ya sababu za hatima ya maisha yao. Mwandishi anayaonesha haya ili kudhihirisha uhalisi wa fikra za jamii yake kama sampuli ya jamii za Kiafrika. Makala hii inahitimisha kuwa fasihi andishi inahifadhi na kuonesha maarifa yanayoisawiri jamii husika.
  • Item
    Usawiri wa eskatolojia ya Waafrika katika mbolezi za Wangoni
    (CHALUFAKITA 2020, JUZ. NA. 2, 2020) Duwe, Martina
    Eskatolojia ni kipengele kimojawapo kinachodhihirisha falsafa ya jamii za Waafrika kulingana na mila na desturi zao. Tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu dhana hii zimejiegemeza katika muktadha wa kiteolojia. Baadhi ya tafiti hizo ni zile zilizofanywa na Baloyi (2008) na Lup (2013). Licha ya kuwapo kwa tafiti hizo, dhana ya eskatolojia ya Waafrika hususani fasihi simulizi za jamii ya Wangoni bado haijamakinikiwa ipasavyo. Aidha, ni wazi kwamba fasihi simulizi ni fasihi inayobeba na kuibua maarifa ya kifalsafa yanayoisawiri jamii husika kulingana na kaida zao. Kwa mantiki hiyo, makala hii inajadili usawiri wa eskatolojia ya Waafrika katika kipera cha mbolezi hususani za jamii ya Wangoni ili kubainisha maarifa yanayobebwa katika kipera hicho. Makala hii ni matokeo ya utafiti uliofanyika kwa kutumia mbinu ya ushuhudiaji shirikishi katika matukio yanayoambatana na suala la kifo na mahojiano ya ana kwa ana na baadhi ya Wangoni katika mazingira yao halisi. Data zimechanganuliwa kwa njia ya maelezo. Data hizo zinaonesha kuwapo kwa eskatolojia ya Waafrika katika mbolezi za jamii hiyo. Hata hivyo, makala hii inajadili vipengele muhimu vitatu tu ambavyo ni: kuamini katika uwepo wa Mungu, mwendelezo wa maisha baada ya kifo na nguvu za waliokufa (mizimu).