Research Papers
Permanent URI for this collectionhttps://scholar.mzumbe.ac.tz/handle/123456789/1446
Browse
4 results
Search Results
Item Mitazamo ya Waafrika kuhusu urithishwaji wa mali: Uchunguzi wa bunilizi za Kiswahili(Mwanga wa Lugha, 2024) Duwe Martina; Fuluge AdriaKurithisha mali katika jamii nyingi za Kiafrika ni suala linalohifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii. Hivyo, thamani ya mwanadamu katika ulimwengu wake hubainika pia kupitia mali anazorithisha wengine. Vilevile, kupitia mali hizo, mrithishaji anaendelea kuishi katika fikra za wanaorithishwa hata baada ya kifo chake. Kwa msingi huo, urithishwaji wa mali ni hazina inayoendeleza kizazi na kuleta kumbukumbu idumuyo katika ulimwengu halisi wa mwanadamu. Fasihi ni akiso la maisha ya mwanadamu katika mazingira yake halisi. Kwa mantiki hiyo, bunilizi za Kiswahili huhifadhi na kudokeza misingi mbalimbali inayozingatiwa katika kuendesha maisha ya jamii. Mathalani, ile inayohusu suala la urithishwaji wa mali kupitia wahusika wanaosukwa kwa ustadi unaokidhi haja ya kufikisha maudhui lengwa. Hata hivyo, haijaelezwa bayana mitazamo ya Waafrika kuhusu suala la urithishwaji wa mali kwa kuhusianisha na bunilizi za Kiswahili. Hivyo basi, makala hii imeshughulikia jambo hilo kwa kujiegemeza katika riwaya za Rosa Mistika (1971) na Dunia Uwanja wa Fujo (1975). Makala hii ni matokeo ya data zilizopatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji. Vilevile, katika uchunguzi, uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo hayo, misingi ya Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi imetumika. Matokeo yanaonesha kuwa katika suala la urithishwaji wa mali kwa Waafrika, kuna mitazamo mbalimbali inayozingatiwa. Makala hii inajadili mitazamo mikuu mitatu, ambayo ni: mtazamo wa kitamaduni, kihiari, na kimabavu.Item Viashiria vya kujiua: Uchunguzi wa mhusika kazimoto katika riwaya ya kichwamaji(Journal of Kiswahili and Other African Languages, 2024) Fuluge, AdriaWahusika katika kazi za fasihi huumbwa kwa ustadi mkubwa kwa lengo la kubeba tafakuri na fikra za mtunzi kuhusu maisha ya jamii. Katika uumbaji huo, aghalabu, binadamu husawiriwa kama kiumbe anayeteseka na anayeishi katika ulimwengu usiomjali, aliyezungukwa na mateso na ubwege1, na anayeshindwa kukabiliana vyema na uhalisia wake (Wamitila, 2002). Mambo hayo, ndiyo huweza kusababisha afanye maamuzi fulani kama vile kujiua. Hivi ndivyo anavyofanya Euphrase Kezilahabi katika riwaya ya Kichwamaji (1974) anapomuumba mhusika anayejiua.Hata hivyo, kwa kuwa kujiua huambatana na viashiria mbalimbali, makala haya yanajadili viashiria vya kujiua kwa mhusika mkuu katika riwaya teule tu. Riwaya hiyo imeteuliwa kwa sababu ina mawanda ya kutosha yaliyowezesha kupata data zilizolengwa katika makala haya. Pia, riwaya hiyo imeteuliwa kama sampuli ya kuwakilisha riwaya nyingine zenye viashiria vya kujiua. Misingi ya Nadharia ya Udhanaishi imetumika katika uchunguzi, uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa matini. Mjadala umebainisha kwamba katika riwaya ya Kichwamaji vipo viashiria vinne vya kujiua vilivyomkumba Kazimoto kabla ya kujiua kwake. Viashiria hivyo ni kukata tamaa, kujitenga kijamii, kuzungumzia masuala ya kujiua na mabadiliko ya tabia. Makala yanahitimisha kwamba jamii inahitaji kupewa elimu ya kutosha kuhusu kujiua kwa wahusika pamoja na viashiria vyake ili iweze kumtambua na kumsaidia mtu mwenye viashiria vya kujiua.Item Hatima ya maisha ya Waafrika katika Bunilizi za Kiswahili: Mwegamo wa kifalsafa(Ruaha Journal of Arts and Social Sciences (RUJASS), 2021) Duwe, MartinaMakala hii imefafanua sababu za hatima ya maisha ya mwanadamu kulingana na fikra za Waafrika kwa kurejelea riwaya za Utengano (1980) na Tata za Asumini (1990). Data za msingi zilizofafanuliwa katika makala hii zimepatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji makini. Nadharia ya Udhanaishi imetumika kama mwegamo muhimu katika uchambuzi na mjadala wa data zilizowasilishwa katika katika utafiti uliofanyika. Matokeo yanaonesha kuwa utajiri wa maarifa yaliyomo ndani riwaya teule husawiri maudhui na fikra halisi za Waafrika kulingana na tamaduni zao. Fikra hizo hudhihirisha falsafa inayotawala maisha yao. Pia, hubainisha sababu mbalimbali za hatima ya mwanadamu kulingana na mitazamo ya Waafrika. Kifo ni miongoni mwa sababu zilizobainika wazi katika riwaya teule kuwa kinasababishwa na maamuzi ya Mungu, maovu ya mwanadamu mwenyewe na watu wanaomzunguka katika mazingira yake halisi; na namna Waafrika wanavyofikiri juu ya sababu za hatima ya maisha yao. Mwandishi anayaonesha haya ili kudhihirisha uhalisi wa fikra za jamii yake kama sampuli ya jamii za Kiafrika. Makala hii inahitimisha kuwa fasihi andishi inahifadhi na kuonesha maarifa yanayoisawiri jamii husika.Item Usawiri wa eskatolojia ya Waafrika katika mbolezi za Wangoni(CHALUFAKITA 2020, JUZ. NA. 2, 2020) Duwe, MartinaEskatolojia ni kipengele kimojawapo kinachodhihirisha falsafa ya jamii za Waafrika kulingana na mila na desturi zao. Tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu dhana hii zimejiegemeza katika muktadha wa kiteolojia. Baadhi ya tafiti hizo ni zile zilizofanywa na Baloyi (2008) na Lup (2013). Licha ya kuwapo kwa tafiti hizo, dhana ya eskatolojia ya Waafrika hususani fasihi simulizi za jamii ya Wangoni bado haijamakinikiwa ipasavyo. Aidha, ni wazi kwamba fasihi simulizi ni fasihi inayobeba na kuibua maarifa ya kifalsafa yanayoisawiri jamii husika kulingana na kaida zao. Kwa mantiki hiyo, makala hii inajadili usawiri wa eskatolojia ya Waafrika katika kipera cha mbolezi hususani za jamii ya Wangoni ili kubainisha maarifa yanayobebwa katika kipera hicho. Makala hii ni matokeo ya utafiti uliofanyika kwa kutumia mbinu ya ushuhudiaji shirikishi katika matukio yanayoambatana na suala la kifo na mahojiano ya ana kwa ana na baadhi ya Wangoni katika mazingira yao halisi. Data zimechanganuliwa kwa njia ya maelezo. Data hizo zinaonesha kuwapo kwa eskatolojia ya Waafrika katika mbolezi za jamii hiyo. Hata hivyo, makala hii inajadili vipengele muhimu vitatu tu ambavyo ni: kuamini katika uwepo wa Mungu, mwendelezo wa maisha baada ya kifo na nguvu za waliokufa (mizimu).