Abstract:
Tasinifu hii ni matokeo ya utafiti wenye mada inayoitwa -Usawiri wa Matukio ya Mchakato wa Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi: Ni Mwangwi wa Mtanziko wa Kijamii?‖ Lengo kuu lilikuwa kuchunguza usawiri wa matukio ya kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi kama ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii, au la. Malengo mahususi yaliyoshughulikiwa ni matatu: Mosi, kubainisha usawiri wa matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi; pili, kubainisha sababu za mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika riwaya teule; na tatu, kutathmini uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii. Ili kuyafikia malengo hayo, mbinu za aina mbili zilitumika katika mchakato wa ukusanyaji wa data. Mbinu ya kwanza ilikuwa ni ukusanyaji wa data za maktabani kwa kusoma na kuchambua kwa makini matini teule na magazeti mbalimbali yenye taarifa zinazohusiana na mada ya utafiti. Pili, ilikuwa ni mbinu ya mahojiano na watafitiwa iliyotumika kukusanya data za uwandani. Kimsingi, shughuli nzima ya ukusanyaji wa data, uchanganuzi wake, na suala la kutafsiri matokeo ya utafiti ilikitwa katika mkabala wa kitaamuli. Data hizo zilihakikiwa, kuchanganuliwa na kupangwa katika mada ndogondogo kulingana na namna zinavyooana kimaudhui. Nadharia za Udhanaishi na Sosholojia ya Kifasihi ndizo zilizomwongoza mtafiti katika mchakato wa uchambuzi wa data zake.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba, matukio yanayosawiriwa katika riwaya teule ndiyo yaliyounda mchakato wa kujiua kwa wahusika. Katika riwaya ya Rosa Mistika matukio hayo yanamhusu Rosa Mistika; nayo ni: kupigwa na baba yake, kuwachongea wasichana wenzake, kuota ndoto, kusimamishwa shule, kufumaniwa na kufukuzwa chuo. Mengine ni kutoa mimba, kujitenga na kutengwa na jamii yake, na kuachwa na mchumba wake. Kwa upande wa riwaya ya Kichwamaji matukio hayo yanayohusu kujiua kwa Kazimoto ni: kunyimwa kazi, Rukia kutiwa mimba, vifo vya Rukia na mama yake, na kifo cha Kalia. Matukio mengine ni kifo cha mtoto wake, kuugua ugonjwa wa ajabu, na kujitenga kijamii. Matukio mengine ya kujiua yanasawiriwa katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo na yanamhusu Tumaini, yaani matukio ya aibu na fedheha, na tukio la Tumaini kumuua Mkuu wa Wilaya. Pia, sababu mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, na kifalsafa, zimebainika kuwa chanzo cha mtu kupata mitanziko ya kimaisha. Mitanziko hiyo husababisha mtu huyo kuwa katika mkinzano wa mawazo, ambayo humpa wakati mgumu wa kuamua la kufanya, kwa kuwa uamuzi wowote kwake huwa na madhara. Aidha, utafiti umebaini kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya matukio ya mchakato wa kujiua yaliyomo katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii vii kwa jumla. Uhusiano huo umebainishwa na kuwekwa katika makundi mawili. Mosi, uhusiano wa sababu za matukio ya kujiua, ambazo ni kujiua kunakosababishwa na athari za mahusiano ya kimapenzi, kujiua kunakosababishwa na athari katika malezi na migogoro ya kifamilia, na kujiua kunakosababishwa na athari za magonjwa. Pili, uhusiano wa njia zinazotumika katika kujiua. Njia hizo ni kujiua kwa kujinyonga, kujipiga risasi, kujichoma kisu, na kwa kutumia sumu.
Mchango mpya wa utafiti huu ni pamoja na: Mosi, kubainishwa kwamba kujiua ni mchakato na siyo tukio la ghafla kama ilivyofahamika awali kupitia tafiti zilizotangulia miongoni mwa wanajamii. Pili, kuleta mtagusano wa kitaaluma kwa kuzishikamanisha nyuga mbalimbali, zikiwamo Afya, Saikolojia, Sosholojia, na Fasihi. Tatu, kinadharia na kiuchambuzi ambapo licha ya kuendeleza nadharia ya Udhanaishi iliyozoeleka katika uchambuzi wa riwaya teule, nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi pia imetumika. Nne, kwa watunga sera na wakuza mitalaa kuweza kuchukua hatua madhubuti na za pamoja katika kulishughulikia tatizo la watu kujiua ili lisiendelee kuzikumba na kuziathiri jamii zetu.