Abstract:
Pamoja na kwamba lugha ya Kiswahili ina maneno mengi yaliyokopwa katika lugha
ya Kiarabu, haijawa wazi ni kwa namna gani maneno hayo (hasa vitenzi) ya
Kiswahili yenye asili ya Kiarabu yamepata sifa za Kibantu. Kwa hiyo, kuna masuala
kadhaa kuhusu ubantuishaji wa vitenzi vya mkopo ambayo hayajawa wazi. Masuala
hayo ni kama vile ubainishaji wa maumbo ya vitenzi, ufafanuzi wa michakato ya
kimofolojia inayopitiwa katika ubantuishaji wa vitenzi hivyo, na tathmini ya
mwelekeo wa ubantuishaji wa vitenzi hivyo. Utafiti ulifanyika katika Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania, ambapo ulihusisha maeneo ya Tanzania bara na Zanzibar.
Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa njia tatu ambazo ni: upitiaji wa nyaraka, usaili
na upimaji wa usahihi wa kisarufi. Katika uchanganuzi na ufasiri wa data, Nadharia
ya Mofolojia Leksika na Nadharia ya Usarufishaji zilitumika. Matokeo ya utafiti huu
yanaonesha kuwa, msambao wa vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu katika
ruwaza ya vitenzi vya Kibantu unachukua maumbo kumi (10) kati ya kumi na moja
(11) ya ruwaza hiyo sawa na vitenzi vya Kiswahili asilia. Tofauti kubwa ya vitenzi
vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu imebainika katika baadhi ya michakato ya
ubantuishaji ya vitenzi hivyo. Vilevile, viambishi vya vitenzi vimechanganuliwa
katika darajia nne zenye kuakisi michakato ya unyambuzi au uambatizi wa viambishi
husika. Darajia hizi pia zinaakisi viwango vya ukale wa viambishi vya Kiswahili.
Ukale huo umepimwa kwa enzi za kabla ya Kiswahili kukutana na Kiarabu. Baadhi
ya viambishi visivyojitokeza katika vitenzi vyenye asili ya Kiarabu ni vyenye ukale
wa zamani zaidi, na kwamba michakato yake kimofolojia na kifonolojia ilishakoma
kabla Kiarabu kukutana na Kiswahili. Pia, vitenzi vilivyochanganuliwa kimofolojia,
mwelekeo wake wa ubantuishaji umebainika kwa kutumia Nadharia ya Usarufishaji.
Kutokana na nadharia hiyo, ukamilifu na usiukamilifu wa ubantuinshaji wa vitenzi
hivyo umebainishwa. Ukamilifu na usiukamilifu umebainika kutokana na matumizi
ya ruwaza ya vitenzi vya Kibantu na michakato ya ubantuishaji. Kwa kuwa utafiti
huu umechunguza vitenzi vya Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu, tafiti zijazo
zinaweza kuchunguza aina nyingine za maneno. Hata hivyo, kwa kuwa usarufishaji
hufanyika taratibu halikutolewa hitimisho la kuonesha ubantuishaji wa vitenzi vya
Kiswahili vyenye asili ya Kiarabu unapokomea.